Hapa na Pale
Baraza la Usalama limeinasihi Serikali ya Sudan, pamoja na makundi yote yaliohusika na mgogoro wa Darfur, kushikirkiana kikamilifu, halan, na Mahakama ya Kimataifa juu ya Jinai ya Halaiki (ICC); na kuhakikisha pia wale waliowajibika na makosa ya vita katika eneo la Darfur kuwa wanafikishwa mahakamani kukabili haki, bila ya kuchelewa.~
Kadhalika, Jaji wa Tawi la Mahakama ya ICC kunapozingatia kesi ya Thomas Lubanga Dyilo, aliyekuwa kamanda wa waasi katika JKK (DRC), ameamua kusimamisha uendeshaji wa mashitaka baada ya kubainika kwamba Mwendesha Mashitaka alificha nyaraka za siri za ushahidi zaidi ya 200, nyaraka ambazo zingelifichuliwa zingelisaidia kuthibitisha wazi ya kuwa mtuhumiwa Lubanga alikuwa hana hatia na hahusiki na mashitaka. Hivi sasa Mahakama inajitayarisha mnamo Juni 24 kusikiliza kesi ya kumwachia huru Lubanga kutokana na taarifa hizo.
Ijumatatu, Juni 16 (2008) katika mji wa London KM Ban Ki-moon alishiriki kwenye taadhima maalumu za kuheshimu na kukumbuka mchango wa wale waandishi habari wa kimataifa waliouawa wakati wakiendeleza majukumu yao, watu ambao alisema walikuwa wakijaribu kuwapatia sauti wasiokuwa na kauli, kwa kufungamana na uhuru halali wa vyombo vya habari wa kuchunmguza na kutafuta habari kwa manufaa ya umma. Kwenye taadhima hizo, kulifunuliwa mnara maalumu uliotengenezewa glasi na chuma, uliopewa jina lisemalo "Uvutaji Hewa Safi", sanamu ambalo kwa muda wa nusu saa kila siku usiku, humurika na kuangaza angani mwenge wa kilomita moja, ikiwa kama ni kumbukumbu ya wanahabari waliopoteza maisha wakati wakitekeleza shughuli zao za kikazi.
Kuanzia tarehe 17 hadi 21 Juni watoto 700 wa umri wa kati ya miaka 10 mpaka 14, kutoka nchi 100 ziada, wamekusanyika kwenye mji wa Stavanger, Norway kuhudhuria mkutano wa UM wenye makusudio ya kusailia mchango wa vijana hawa katika kuleta mageuzi ya mazingira yenye natija kwa umma wa kimataifa. Kikao cha mwaka huu, kiliandaliwa bia bia na shirika la UM juu ya maendeleo ya watoto, UNICEF, na pia ile taasisi inayohusika na hifadhi ya mazingira, UNEP pamoja na shirika lisio la kiserekali la Norway linaloitwa Ajenda 21 ya Vijana, wakati Mkutano ukiendelea kufadhiliwa, vile vile, na mchango wa kampuni ya kimataifa ya madawa ya Bayer AG.