Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Baraza la Usalama limekutana kusailia na kushauriana juu ya operesheni za Shirika la UM linalosimamia usitishwaji wa mapigano mipakani Ethiopia na Eritrea (UNMEE), na pia kuzingatia hatua za kuchukuliwa siku za mbele na jamii ya kimataifa kuhusu ulinzi wa eneo hilo.

Timu ya watumishi wakaazi wa UM waliopo Afrika Kusini imeripotiwa wanashirikiana na Serikali kuisaidia kudhibiti vizuri zaidi huduma za kukidhi mahitaji ya wageni wahamiaji, kufuatilia mifumko ya karibuni ya fujo na vurugu liliochochewa na chuki za wageni. Kadhalika, Shirika la UNHCR limeanzisha huduma maalumu ya simu maalumu ya kutumiwa na wahamiaji pamoja na wale wageni walioomba hifadhi ya kisiasa Afrika Kusini, kupatiwa misaada ya haraka pakizuka dharura. Halkadhalika, UNHCR inaisaidia Serikali ya Kenya kusajili wahamiaji waliopo katika Jimbo la Gauteng. Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo ya Watoto (UNICEF) nayo kwa upande wake ipo mashughuli kusaidia watoto wahamiaji kupatiwa hifadhi na ulinzi unaofaa, elimu na lishe bora.

Timu ya wataalamu wa Shirika la UM juu ya Matumizi ya Amani ya Nishati ya Nyuklia (IAEA) imewasili Syria mwisho wa wiki iliopita kuendeleza uchunguzi kuhusu ukweli wa taarifa zilizopokelwa zinazodai karkhana ilioharibiwa na makombora ya Israel ndani ya Syria Septemba ya mwaka jana ilikuwa mtambo wa kutengenezea nyuklia ambao bado haukuanzishwa shughuli zake.