Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

BU kushtumu fujo na utumiaji mabavu Zimbabwe

BU kushtumu fujo na utumiaji mabavu Zimbabwe

Ijumatatu usiku, Baraza la Usalama liliafikiana, kwa kauli moja, kushtumu kampeni ya utumiaji mabavu inayoendelezwa na wenye madaraka Zimbabwe, dhidi ya wapinzani wa kisiasa, na pia kulaani vitendo vya Serikali ambavyo inaripotiwa huwanyima wapinzani haki ya kuendeleza kampeni huru za uchaguzi. Kwenye taarifa iliotolewa baada ya majadiliano ya faragha katika Baraza la Usalama, Raisi wa mwezi Juni wa Baraza, Balozi Zalmay Khalilzad wa Marekani alisema wajumbe wa Baraza wanaamini fujo iliotanda sasa hivi Zimbabwe, ikichanganyika na vikwazo dhidi ya vyama vya upinzani, ni hali ambayo uchaguzi ulio huru na wa haki hauwezekani kufanyika abadan, uchaguzi ambao umetayarishwa ufanyike Juni 27 (2008).

Kadhalika ilitakiwa iwaachie viongozi wa kisiasa wapinzani walio vizuizini. Halkadhalika, Baraza limeshtumu uamuzi wa Serikali ya Zimbabwe kusitisha operesheni za kuhudumia misaada ya kiutu nchini humo, na kuwanasihi wenye Serikali kuzirudisha tena kadhia hizi mapema iwezekanavyo. Vile vile Baraza la Usalama limesisitiza waangalizi wa kimataifa waliopo Zimbabwe waendelee kubakia nchini kuendeleza shughuli zao, licha ya kuwa mgogoro bado umeselelea.