Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Baraza la Usalama, kwenye taarifa ya raisi kwa mwezi Juni, limeyasihi makundi yote yanayohasimiana Sudan Kusini kutumia mwongozo wa \'ramani ya mapatano\' yaliofikiwa Juni 8 kwenye yale Maafikiano ya Jumla ya Amani, ili kuzima cheche za fukuto liliozusha fujo za karibuni kwenye mji wa Abyei.

Ripoti mpya ya KM juu ya hali katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na shughuli za Ofisi ya Kusaidia Kuimarisha Ujenzi wa Amani inasema hali huko ya kisiasa, usalama na masuala ya uchumi na jamii ni bado ya kuregarega, kwa ujumla. Alisema taswira hiyo imeghumiwa na ufukara uliotanda, pamoja na ukosefu wa utulivu, ikichanganyika na duru ya kusikitisha ya ukiukaji wa haki za binadamu unaoendelezwa na watu wasiojali adhabu. Makundi ya waasi wenye kuchukua silaha yalinasihiwa kuzisalimisha silaha zao, na pia kutakiwa washirikiane kwa pamoja kwenye juhudi za kurudisha utulivu na amani kitaifa.

Kadhalika KM aliwakilisha ripoti nyengine kuhusu hali ya watoto walionaswa katika mazingira ya vita na uhasama Uganda, ambayo ilielezea fafanuzi za Joaquim Chissano, Mjumbe Maalumu wa UM kwa Eneo la Uganda lilioathirika na mashambulio ya kundi la waasi wa LRA. Ripoti ilizungumzia masuala kadha muhimu, hususan lile tatizo linalohusu tabia ya kuwalazimisha watoto wasiofikia umri wa utu uzima kushiriki kwenye mapigano na vita, vitendo ambavyo vimepigwa marufuku kimataifa.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limechapisha orodha mpya ya kukagulia usalama na usafi wa zana za kupasulia mahospitalini, orodha itakayotumiwa kuhawasaidia wahudumia afya kuhakikisha upasuaji pote duniani unakuwa salama.

Thoraya Ahmed Obeid, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Mfuko wa Kudhibiti Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) alisema kwamba azimio liliopitishwa kwa kauli moja na Baraza la Usalama karibuni, kwa madhumuni ya kukomesha haraka vitendo vyote vya kutumia mabavu dhidi ya wanawake na watoto wa kike kwenye hali ya mapigano, pendekezo hilo alilifananisha na "mafanikio makubwa ya kihistoria" yatakayosaidia kudumisha hifadhi bora na hishima ya wanawake na watoto wa kike kote duniani.

Kwenye mkutano ulioongozwa na Shirika la UM juu ya Maendeleo ya Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwenye mji wa Casablanca, Morocco kulitiwa sahihi Mradi wa Vitendo wa Mapendekezo 10 miongoni mwa wawakilishi wa kutoka miji saba ya mataifa ya KiArabu, kwa malengo ya kupiga vita vitendo vya ukabila. Miji hii itashikamana kwenye kadhia hizo na mtandao wa miji ya kikanda katika Ulaya, Afrika, Amerika ya Latina na pia Majimbo ya Asia-Pasifiki.