Skip to main content

Taka za elektroniki zahatarisha afya ya umma: UNEP

Taka za elektroniki zahatarisha afya ya umma: UNEP

Achim Steiner, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Hifadhi Mazingira (UNEP)ametoa onyo linalohadharisha walimwengu ya kuwa mamilioni ya zile simu za mkononi na kompyuta zinazotupwa ovyo kwenye majaa ya kimataifa, katika sehemu mbalimbali za dunia, huhatarisha afya ya umma kijumla.

Onyo hilo liliwasilishwa mbele ya kikao cha wajumbe waliohudhuria mkutano wa kuzingatia udhibiti bora wa taka na mabaki ya vifaa na zana za mawasiliano ya kisasa, unaofanyika kwenye mji wa Bali, Indonesia wiki hii. Steiner aliongeza kusema asilimia kubwa ya taka zinazozalishwa na vyombo vya mawasiliano katika nchi tajiri humalizikia kwenye majalala ya nchi masikini ya Afrika na Asia, vifaa ambavyo vikishatupwa na kuchanganyika pamoja na maadini yalio magumu kuyeyuka kwenye ardhi, huanza kuvuja sumu ya kemikali na kuharibu hewa na mazingira. Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) tani milioni 20 hadi 50 za taka za elektroniki hutupwa na kumwagwa ulimwenguni kila mwaka.