Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamishna wa Haki za Binadamu anawatetea wadhaifu wa kimataifa kupata chakula

Kamishna wa Haki za Binadamu anawatetea wadhaifu wa kimataifa kupata chakula

Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Louise Arbour jana Alkhamisi naye pia alijumuisha sauti yake katika kuwatetea wadhaifu wa ulimwengu ambao sasa hivi wanaathiriwa na tatizo la chakula liliopamba dunia, hasa mgogoro uliozushwa na mifumko ya bei za nafaka katika soko la kimataifa. ~

Alisisitiza kwamba masaibu yaliouvaa umma uliotengwa kijamii kwa sababu ya maisha duni, na pia ubaguzi dhidi yao ni masuala yanayowajibika kushughulikiwa haraka ikiwa kweli walimengu tumewania kuutatua mgogoro wa chakula kwa usalama.

Bi Arbour pia alisema anakhofia kuwa pindi tutashindwa kuudhibiti mgogoro huu wa chakula kuna hatari ya kuzuka machafuko ambayo huenda yakaathiri pia zile haki nyengine za kibinadamu, mathalan huenda ikaathiri uhuru wa raia kutoa mawazo na kujieleza, na kusitisha uhuru wa watu kukusanyika bila ya kutishiwa na vikosi vya usalama vya wenye mamlaka.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu alimaliza risala yake kwa kuihimiza jamii ya kimataifa kuzipa usikizi unaofaa sauti zote za umma, kutoka kila tabaka – ama kusikiliza moja kwa moja kutoka midomo yao au kwa kupitia jumuiya za kiraia – hatua ambayo huenda ikatupatia mafanikio katika juhudi za kudhibiti matatizo ya chakula, kwa natija za wote.