Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma za kihali za UM Myanmar kuongeza kasi

Huduma za kihali za UM Myanmar kuongeza kasi

Ijumanne mashirika ya UM yanayohudumia misaada ya kiutu yalifanyisha mkutano na waandishi habari Geneva kuelelzea hali, kwa sasa, katika Myanmar, baada ya taifa hilo kupigwa na dhoruba kali ya Kimbunga Nargis Ijumaa iliopita.

Shirika linalohudumia watoto, UNICEF, limeripoti ya kuwa wanawake na watoto katika Myanmar hujumuisha asilimia 60 ya idadi ya watu nchini na inakhofiwa kuwa hili ndio fungu kubwa la raia waliodhurika zaidi na maafa ya kimbunga. UNICEF itaongoza kwenye shughuli za kuwapatia watu maji safi, na usafi wa makazi, na pia kuhakikisha watoto wanapewa hifadhi bora na wanaendelea kuilimishwa kama inavyopasa.

Wafanyakazi wakaazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) waliopo Myanmar wanakhofia kwamba pindi hali ya afya haijadhibitiwa mapema kuna hatari ya kufumka maradhi hatari ya kuambukiza nchini, yanayosababishwa na maji, mathalan, Ugonjwa wa Kuharisha, Kipindipindu na Malaria.

Mashirika kadha mengineyo ya kimataifa yamejumuika kuchangia katika kusaidia kihali umma wa Myanmar, miongoni mwao likiwemo Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC), ambalo wafanyakazi wake wanashiriki hivi sasa kwenye juhudi za kufarajia na kugawa misaada ya dharura kwa waathiriwa husika – watu milioni moja wanakadiriwa kukosa makazi.

Alasiri Shirika la IFRC limetoa ombi maalumu lilioitaka jumuiya ya kimataifa kuchangisha haraka msaada maridhawa wa fedha zinazohitajika kunusuru maisha ya mamilioni ya umma katika Myanmar ambao sasa hivi umekabiliwa na msiba wa Kimbunga Nargis.