UM inakithirisha huduma za kiutu Myanmar kufuatia Kimbunga Nargis

UM inakithirisha huduma za kiutu Myanmar kufuatia Kimbunga Nargis

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti kwamba ndege iliochukua tani 25 za metriki za vifaa vya kuhudumia mahitaji ya dharura, iliwasili Yangon, Myanmar Alkhamisi. Hii ni ndege ya kwanza ya UM kuruhusiwa kuingia nchini humo, na kufuatiwa baadaye na ndege nne nyengine, ambazo zimeshatayarishwa kupeleka misaada ziada inayohitajika kuhudumia umma ulioathirika na Kimbunga Nargis kilichopiga Myamar karibuni.~Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti wataalamu wanne wanaowakilisha timu ya UM ya Kutathminia Mahitaji Halisi ya Umma Penye Maafa Maumbile nao pia wanajianda kwa hivi sasa kuelekea Myanmar kuendeleza ukaguzi wao.~

Shirika la UM juu ya Maendeleo ya Watoto (UNICEF), kwa upande wake, limeripoti kuwa na wasiwasi mkuu kuhusu afya ya watoto walionaswa kwenye maeneo ya nchi yalioharibiwa na Kimbunga Nargis. UNICEF ilikumbusha ya kuwa watoto ndio fungu kubwa la raia ambao hudurika mapema pakizuka maafa, na wanahitajia kupatiwa huduma za kwanza za afya dhidi ya maradhi ya kuambukiza, haraka iwezekanavyo. Hivi sasa meli mbili zilizokodiwa na UNICEF ziko njiani kuelekea Myanmar, zikibeba vifaa maalumu vya kukidhi mahitaji ya dharura ya umma ulioathirika na uharibifu wa Kimbunga Nargis, mathalan, madawa, tembe za kusafishia maji ya kunywa, maturubali ya kuzindikia makazi ya muda, vyandarua na vifaa vyengine muhimu vya kunusuru maisha.