Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP inaomboleza mauaji ya mtumishi mwenzi Kenya kaskazini

WFP inaomboleza mauaji ya mtumishi mwenzi Kenya kaskazini

Shirika la WFP limethibitisha kwamba majambazi wasiotambulikana, Ijumatano walimpiga risasi na kumwua Silence Chirara, Mkuu wa ofisi ndogo ya WFP iliopo katika kaskazini-magharibi ya Kenya katika mji wa Lokichoggio, ambapo WFP huongozea operesheni za kupeleka misaada ya kiutu kwa Sudan kusini. Kwa mujibu wa WFP kitendo hiki ni cha kikatili na kinalaaniwa kwa kauli nzito kabisa na UM. Silence Chirara alikuwa mratibu wa operesheni za WFP katika eneo hilo. Mpaka sasa haijajulikana kiini hasa cha majambazi kumdunga risasi marehemu Chirara. Wafanyakazi wa usalama wa UM wakishirikiana na polisi Kenya wameshaanzisha upelelezi wa kuwasaka maharamia waliohusika na mauaji hayo ya marehemu Chirara, aliye raia wa Zimbabwe.