Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Myanmar yanasihiwa kurahisisha huduma za kiutu kwa umma muathiriwa

Myanmar yanasihiwa kurahisisha huduma za kiutu kwa umma muathiriwa

Noeleen Heyzer, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya UM juu ya Maendeleo ya Kiuchumi na Jamii katika Asia (ESCAP) ametoa mwito maalumu wenye kuwahimiza wenye mamlaka katika Myanmar kusaidia mashirika ya kimataifa kurahisisha, na kuharakisha, huduma za ugawaji wa misaada ya kiutu kwa wale waathiriwa wa Kimbunga Nargis milioni 1.5 wanaokadiriwa kusumbuka zaidi na ambao wanategemea haraka misaada hiyo kunusuru maisha. Alisisitiza hali katika Myanmar hivi sasa ni ya kutia "wasiwasi mkubwa na inahuzunisha" kwa sababu ya kucheleweshwa kwa shughuli za ugawaji wa misaada ya dharura, hususan kwenye yale maeneo yaliotenguka kijamii baada ya miundombinu yao kuharibiwa na kuangamizwa na tofani iliopiga nchini wiki iliopita.~

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limo mbioni kutafuta usafiri mbadala kuharakisha huduma za kupeleka tani 57 za vifaa vya makazi ya muda vitakavyotumiwa kuwapatia umma muhitaji katika Myanmar. Vifaa hivi vitasafirishwa kutoka ghala za UM ziliopo Dubai.

Kadhalika, Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti kwamba limeshiandaa kupeleka Myanmar ndege mbili zaidi zitakazobeba shehena ya misaada ya dharura itakayokidhi huduma za kwanza kwa raia walioathirika na Kimbunga Nargis. Wakati huo huo WFP imeeleza kuwa itaendelea na mazungumzo ya ushauri na wenye mamlaka Myanmar juu ya hatua za kuchukuliwa shirika, ili kuhakikisha ugawaji wa misaada ya kihali unawafikia walengwa.