Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bei kubwa za chakula zitaendelea kuselelea miaka ijayo,FAO yaonya

Bei kubwa za chakula zitaendelea kuselelea miaka ijayo,FAO yaonya

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) kwenye ripoti ya mwaka iliotayarishwa bia na Shirika la la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) kubashiria Matarajio ya Kilimo duniani imethibitisha kwamba bei za bidhaa za kilimo kwenye soko la kimataifa zitaendelea kuwa za kigeugeu katika kipindi kijacho.

Ripoti imeashiria, kwa kulingana na matokeo ya utafiti wa taasisi za FAO na OECD, ya kwamba katika miaka 10 ijayo bei za chakula zitapanda kwa kiwango kitakachokiuka bei wastani za miaka kumi iliopita. Ripoti ilisema umma utakaoteswa zaidi na mifumko ya bei za chakula utakuwa wale watu wenye kuishi kwenye miji, pamoja na wanavijiji wasio wakulima, hususan katika yale mataifa yenye mapato madogo.

FAO imeihimiza UM na mashirika yake kuandaa, haraka, miradi ya dharura itakayoiwezesha jamii ya kimataifa kukabiliana vyema na hali hii ya hatari, na kujizatiti vilivyo kwenye juhudi za kutafuta suluhu ya kudumu itakayohakikisha tatizo kama hili la chakula halitozuka tena. FAO imesisitiza kuwa ni muhimu kwa Mataifa Wanachama kukithirisha uwekezaji katika sekta kilimo, hasa kwenye nchi zinazoendelea ili kudhibiti bora matatizo ya kupanda kwa kasi kwa bei za chakula katika masoko ya kimataifa.