Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nini maana ya Siku Kuu ya Walinzi wa Amani Duniani?

Nini maana ya Siku Kuu ya Walinzi wa Amani Duniani?

Kila mwaka, tarehe 29 Mei huadhimishwa na UM kuwa ni Siku Kuu ya Kuheshimu Mchango wa Walinzi wa Amani Duniani. Taadhima za mwaka huu zinawakilisha miaka 60 tangu operesheni za ulinzi wa amani za UM kuanzishwa rasmi mnamo tarehe 29 Mei 1948. KM Ban Ki-moon kwenye risala ya kuiheshimu siku hiyo aliwapongeza walinzi wa amani wa kimataifa, waume kwa wake, waliotawanyika katika sehemu mbalimbali za dunia, kwa mchango wao katika kuimarisha utulivu na usalama wa kimataifa.~

Wakati wa kipindi ambapo mvutano wa Vita Baridi ulishtadi katika uhusiano wa kimataifa, kwa sababu ya itikadi za kisiasa tofauti, Baraza la Usalama lilizirai kikazi na lilishindwa kuyatekeleza majukumu ya kuimarisha usalama na amani ya kimataifa kama ilivyokusudiwa na Mkataba wa UM. Kwa hivyo operesheni za amani za UM kwa wakati huo, zilidhibitiwa katika shughuli za kusimamia ukomeshaji wa mapigano na kusawazisha utulivu utakaoyapatia mataifa yaliofarakana, mwanya wa kusuluhisha mizozo yao ya kisiasa kwa mazungumzo ya amani. Shughuli hizo zilimaanisha UM ulitakikana upeleke waangalizi wa kijeshi pamoja na vikosi vilivyochukua silaha khafifu, ambao jukumu lao hasa lilikuwa ni kuchunguza namna maazimio ya kusitisha mapigano yanavyotekelezwa ardhini na makundi yaliohasimiana na baadaye kuripoti Makao Makuu. Operesheni hizo vile vile zilidhaminiwa madaraka ya kujenga hali ya kuaminiana miongoni mwa makundi yanayohasimiana kwa makusudio ya kuimarisha mapatano ya amani baada ya mapigano kukomeshwa.

Lakini baada ya Vita Baridi kumalizika, mifumo ya shughuli za ulinzi wa amani za UM nayo pia ilibadilika, kwa kiwango kikubwa kabisa, hali ambayo iliilazimisha UM kujihusisha kwenye majukumu mapya kikazi, yaliokuwa na mielekeo ya aina nyingi, yaliokusudiwa kuhakikisha kunakuwepo maafikiano ya amani ya jumla kwa wahusika, na kuweka misingi ya kusukuma mbele, na pia kudumisha amani kwenye sehemu hizo za mapambano. Kwa hivyo, walinzi wa amani wa UM hivi sasa hulazimika kutekeleza majukumu anuwai, yalio magumu na mazito, kwa sababu ya mageuzi hayo, mathalan, ulinzi wa amani wa UM hutakiwa ushirikishwe kwenye juhudi za kufufua taasisi za utawala, au kufuatilia utekelezaji wa haki za binadamu kwa raia, na hutakiwa pia urekibishe mifumo ya sekta ya usalama, na vile vile kudhibiti silaha za vita kitaifa, pamoja na kushughulikia uchanguzi wa wanajeshi, na shughuli nyengine za kuwaunganisha wapiganaji waliosalimu amri kwenye maisha ya kawaida.

Tusisahau pia kwamba mifumo ya migogoro nayo pia imebadilika baada ya Vita Baridi kumalizika na baada ya miaka kadha kupita. Operesheni za siku za nyuma za UM za ulinzi wa amani zilikuwa zinahusika zaidi na shughuli za kutatuta migogoro kati ya mataifa. Siku hizi UM hutumia walinzi wa amani kutenganisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ndani ya taifa. Kadhalika, huduma za ulinzi wa amani za karne ya ishirini na moja huwa zinahitajia sio wanajeshi pekee, bali pia wajuzi wa kiraia waliokuwa na uzoefu wa kusimamia shughuli za utawala. Kwa hivyo, walinzi wa amani wa siku hizi hujumuisha wasomi wa fani ya uchumi na iktisadi, maofisa wa polisi, wataalamu magwiji wa sheria, waangalizi wa uchaguzi, na wale mabingwa wenye ujuzi na umahiri wa kusaka na kufyeka mabomu yaliotegwa ardhini, pamoja na wafuatiliaji wa utekelezaji wa haki za binadamu, na pia wataalamu wanaohusika na masuala ya kiraia na utawala bora, na vile vile wahudumia kadhia za kiutu na mabingwa wa taaluma ya mawasiliano bora ya kisasa yenye natija za umma.

Naibu KM juu ya Operesheni za Ulinzi wa Amani za UM Duniani, Jean Marie-Guehenno katika riasala aliotoa mbele ya waandishi habari wa kimataifa kuadhimisha miaka 60 ya ulinzi wa amani ulimwenguni alionya kwamba licha ya kuwa UM ilifanikiwa kwenye juhudi za kutunza amani, hata hivyo, anaamini bila ya Mataifa Wanachama kupiga moyo konde na kukithirisha michango maridhawa ya fedha kuhudumia ulinzi wa amani, hautofanikiwa kuyakamilisha yale majukumu ya kusawazisha amani kwenye ardhi za maeneo yenye migogoro na mitafaru. Kwa hivyo aliyahimiza Mataifa Wanachama kutopwelewa kuunga mkono juhudi za kisiasa na miradi inayoaminika yenye uwezo wa kuona mbali kimkakati, inayoandaliwa na UM kwa makusudio ya kuharakisha ufufuaji wa amani kimataifa, hususan kwenye maeneo yanayoibuka kutoka yale mazingira ya uhasama, vurugu na mapigano.