Mtazamo wa Mkutano ujao wa Kamisheni ya Udhibiti wa Muongezeko wa Watu na Maendeleo

Mtazamo wa Mkutano ujao wa Kamisheni ya Udhibiti wa Muongezeko wa Watu na Maendeleo

Kuanzia tarehe 07 hadi 11 Aprili Kamisheni ya UM inayohusika na Udhibiti wa Muongezeko wa Watu Duniani na Maendeleo inatazamiwa kukutana kwenye Makao Makuu ambapo wajumbe kutoka Nchi Wanachama 47 watahudhuria kikao chao cha mwaka.

Kwa mujibu wa ripoti ya KM, jumla ya watu wanaoishi kwenye miji hivi sasa ulimwenguni, kwa mwaka 2008, inakadiriwa kufikia watu bilioni 3.4, jumla ambayo kwa mara ya kwanza kihistoria inalingana na idadi ya watu wanaoishi kwenye vijiji. Muongezeko huu mkubwa wa watu wanaohamia mijini, hasa hivi sasa, hukutikana katika nchi zinazoendelea. Ripoti ya KM, ilibainisha kwamba ongezeko la kimaumbile, yaani ziada ya idadi ya watu wanaozaliwa ambayo hukiuka jumla ya vifo, ndio chanzo halisi chenye kupanua kwa wingi mfumko wa wakazi wa mijini, muongezeko ambao ni sawa na asilimia 60 ya wakazi wote wa miji katika nchi masikini.

Ripoti ya KM ilisisitiza pindi uhamiaji wa watu mijini utatunzwa, wale watu wanaohajiri vijijini na mashambani, utatunzwa na kudhibitiwa kama inavyopasa, na utasaidia sana kiuchumi kwa nchi husika, kwa sababu utawafungulia wafanyakazi fursa ya kujihusisha na ajira ya kisasa, yenye uwezo wa kuzalisha pato la kiwango kikubwa ambacho matumizi yake yatachangisha katika kunyanyua sekta nyengine za uchumi.

Kutokana na bayana hiyo ndipo KM aliponasihi kwenye ripoti yake kwamba wenye madaraka wanawajibika kuhakikisha wanatekeleza majukumu muhimu ya kupatia huduma za msingi umma masikini wa mijini, pamoja na wale watu waliopo kwenye miji midogo midogo na katika sehemu za mashambani na vijijini. Huduma hizi zinahusikana na shughuli za utunzaji wa afya, elimu ya msingi, maji safi pamoja na mazingira ya usafi, kadhia ambazo zikikamilishiwa umma zitakuza hali njema na ustawi wa watu na jamii zao.