Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO imehadharisha, upungufu wa chakula ukiselelea duniani machafuko yatashtadi

FAO imehadharisha, upungufu wa chakula ukiselelea duniani machafuko yatashtadi

Jacques Diouf, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Chakula,na Kilimo (FAO) alitoa onyo maalumu hapo Ijumatano wakati alipokuwa anazuru Bara Hindi, ambapo alitahadharisha ya kuwa ulimwengu unawajibika kudhibiti kidharura hatari ya mifumko ya machafuko na vurugu, ambayo huenda ikachochewa na cheche mchanganyiko zinazotokana na kupanda kwa bei ya nishati kwenye soko la kimataifa, pamoja na ongezeko la mahitaji ya chakula duniani, na pia kuenea kwa tibuko la hali ya hewa ya kigeugeu katika ulimwengu, ikijumuika na matumizi ya kihorera ya ardhi ya kulimia kuzalisha nishati ya viumbe hai.

Kwa hivyo, Diouf alihimiza jumuiya kimataifa kuidhibiti hali hii haraka iwezekanavyo kwa masilahi ya umma wa dunia, hasa ule umma unaoishi katika nchi masikini.