Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gharama kuzidi kwa nchi masikini kufidia uingizaji wa nafaka za kigeni, kuonya FAO

Gharama kuzidi kwa nchi masikini kufidia uingizaji wa nafaka za kigeni, kuonya FAO

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limewasilisha ripoti mpya mjini Roma, Utaliana yenye muktadha usemao \'Hali ya Chakula na Matumaini ya Mavuno Duniani\'. Ripoti imebashiria gharama za kuingiza bidhaa za nafaka katika mataifa yanayoendelea zitapanda kwa asilimia 56 katika kipindi cha 2007/2008.

Kuhusu nchi za Afrika zinazokabiliwa na upungufu wa chakula, na kukabwa na pato la kiwango cha chini, ripoti ilibainisha gharama zao za kuingiza bidhaa za nafaka zitapanda kwa asilimia 74, kwa sababu ya muongezeko mkubwa wa karibuni wa bei za nafaka katika soko la kimataifa, pamoja na kuzidi kwa gharama za kusafirishia mizigo, na vile vilekutokana na mifumko ya bei za nishati na mafuta, kwa ujumla, hususan katika miezi miwili iliopita.

Shirika la FAO hivi sasa limeanzisha Mradi wa Dharura Kudhibiti Mfumko wa Bei za Chakula Duniani, mpango unaojulikana kama Mradi wa ISFP, ambao hutumiwa kwenye zile nchi masikini zilizoathirika zaidi na kupanda sana kwa bei za chakula. Mataifa haya hupatiwa misaada ya kiufundi, pamoja na sera mpya ya kilimo itakayowawezesha wakulima wao kuzalisha chakula kwa wingi zaidi na kuhudumia umma kwa utulivu unofaa kihali. Miradi hii hivi sasa inatekelezwa na UM katika baadhi ya nchi za Afrika, ikijumuisha Burkina Faso, Mauritania, Msumbiji na vile vile Senegal.