Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maharamia Darfur wailazimisha WFP kupunguza posho kwa umma muhitaji

Maharamia Darfur wailazimisha WFP kupunguza posho kwa umma muhitaji

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limetangaza leo kwamba kuanzia mwezi ujao wa Mei litalazimika kupunguza kwa nusu, ile posho ya chakula inayopeleka kwenye jimbo la uhasama la Darfur, Sudan kwa sababu malori yalioajiriwa na UM yenye kuchukua shehena ya chakula bado yanaendelea kushambuliwa na maharamia. Vitendo hivi tuliarifiwa huzorotisha sana huduma za kufadhilia misaada ya chakula kwa umma muhitaji katika Darfur.

Kwa mujibu wa ripoti ya WFP, mwaka huu malori 60 yalioajiriwa na WFP yalitekwa nyara na maharamia katika eneo la Darfur; na kati ya jumla hiyo malori 39 yalishindwa kupatikana; na wakati huo huo madereva 26 walioajiriwa na WFP walitoroshwa, na dereva mmoja aliuawa. Mwakilishi Mkaazi wa WFP katika Sudan, Kenro Oshidari alikumbusha kwamba licha ya kuwa Serikali ya Sudan huwasaidia kuwapatia walinzi polisi kufuatana na misafara ya chakula, kwa bahati mbaya kutokana na mashambulio ya mara kwa mara kwenye njia panda za Darfur kumesababisha matatizo katika kuhimili kwa muda mrefu huduma hizi za chakula katika Darfur.