Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

BU na KM washtushwa na vurugu la mauaji Mashariki ya Kati

BU na KM washtushwa na vurugu la mauaji Mashariki ya Kati

Baraza la Usalama (BU) pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon wameshtumu, kipamoja, hali ya kuongezeka kwa vurugu na vurumai katika Tarafa ya Ghaza, lile eneo liliokaliwa kimabavu la Falastina, ambapo darzeni ya raia wameripotiwa kuuawa mnamo siku za karibuni. Kadhalika wapambanaji wa KiFalastina waliokuwa wakirusha makombora ya kienyeji kusini mwa Israel nawo vile vile walishtumiwa.

Kadhalika, Karen Abu Zayd, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia misaada ya kiutu kwa wahamiaji wa KiFalastina (UNRWA) ameripoti “kushtushwa kabisa” na kile alichoelezea kama “ongezeko la vifo vya raia wasio hatia, wakijumuisha watoto wadogo, kutokana na mashambulio ya vikosi vya Israel katika Tarafa ya Ghaza.” Halkadhalika, Mkuu huyo wa UNRWA alishtumu pia urushwaji wa yale makombora ya kienyeji ndani ya Israel unaoendelezwa na wapamabanaji wa KiFalastina.

Ijumatatu, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Binadamu, Louise Arbour alitoa taarifa ilioonyesha kushtushwa binafsi na vurugu liliozagaa Mashariki ya Kati karibuni, na ametoa mwito unaohimiza kuanzishwe, haraka iwezekanavyo, uchunguzi maalumu juu ya vifo vya raia kutokana na mashambulio ya vikosi vya Israel kwenye eneo la Tarafa ya Ghaza.

Kadhalika Ijumatatu Baraza la Usalama limepitisha azimio la kuongeza duru nyengine ya vikwazo dhidi ya Iran, kwa sababu bado inaendelea kuimarisha ule mradi wa kusafisha madini ya yuraniamu (uranium) halisi kuzalisha nishati ya nyuklia, kinyume na mapendekezo ya Baraza ilioitaka Iran isitishe mradi huo. Miongoni mwa vikwazo viliyoekewa Iran ni pamoja ni ruhusa ya kukagua shehena za Iran zilizopigwa marufuku zinaposafirishwa kimataifa, kupeleleza taasisi za fedha za Iran, kunyima haki ya kusafiri baadhi ya viongozi wa taifa hilo na kudhibiti rasilmali zake. Mataifa 14 yalio wanachama wa Baraza la Usalama walitia kura ya upendeleo, hakuna taifa liliotia kura ya upinzani na Indonesia pekee iliamua kutokupiga kura abadani.