Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UM juu ya Huduma za Kiutu anasema amani yahitajika haraka Mashariki ya Kati

Mkuu wa UM juu ya Huduma za Kiutu anasema amani yahitajika haraka Mashariki ya Kati

John Holmes, Naibu KM anayehusika na Masuala ya Kiutu, katika makala alioandika, na kuchapishwa Ijumanne, kwenye gazeti la Misri la Al-Ahram alitahadharisha kwamba pengo linaloendelea kukithiri baina ya malengo ya zile sera za kuleta amani Mashariki ya Kati na ukweli ulivyo kwenye ardhi ya eneo hilo ambapo, alikumbusha, hali bado inaendelea kuharibika kila kukicha, inaweza kutafsiriwa labda matumaini ya amani ya kudumu yametuponyoka, hali ambayo inaweza kurekibishwa haraka pindi jamii ya kimataifa itajizatiti kuchukua hatua za dharura kipamoja za kusuluhisha mzozo huo.

Alisema uamuzi wa kuwatenga wahamiaji wa KiFalastina na maisha ya kawaida, “kutaleta madhara ya kinafsia kwa kundi kubwa la wahamiaji wa zamani duniani.” Karibuni Holmes alitembelea maeneo ya Falastina yaliokaliwa kimabavu, na pia kuzuru Israel, halkadhalika, na alisema mazingira aliyoyashuhudia katika eneo la Tarafa ya Ghaza – ambapo wanaishi WaFalastina milioni 1.5 – yanafanana na “fukuto la shinikizo ya sufuria ya kupikia iliofungwa na kuzibwa kila mahali.”