Tatizo la kiutu linaloisumbua Darfur lazingatiwa na Baraza la Usalama
Ijumanne, Edmond Mulet, Naibu Mshauri wa KM juu ya Operesheni za Ulinzi wa Amani za UM Duniani aliripoti mbele ya Baraza la Usalama maendeleo kuhusu ukamilishaji wa mpango wa kupeleka vikosi mseto vya UNAMID kulinda amani katika jimbo la Darfur. Alionya kwamba jamii ya kimataifa inawajibika kuyashinikiza yale makundi yanayohasimiana katika Darfur, kushirikiana haraka kwenye mazungumzo ya kuleta amani, kabla hali haijaharibika zaidi kieneo.
Baada ya majadiliano kumalizika Raisi wa Baraza la Usalama kwa mwezi Machi, Balozi Vitaly Churkin wa Shirikisho la Urusi alikutana na waandishi habari na kuwaelezea maamuzi ya wajumbe wa Baraza kuhusu Darfur, kama ifuatavyo:
"Wajumbe wa Baraza la Usalama wamedhihirisha wasiwasi mkuu walionao kuhusu hali ngumu ya usalama na matatizo ya kiutu yaliokabili Darfur, kwa hivi sasa. Wanayahimiza makundi yote husika na mzozo huo, kutekeleza mapatano ya kusitisha mapigano, na kujitahidi kujiepusha na vitendo vyote vya uadui, na pia kuheshimu desturi za sheria za kiutu za kimataifa. Kadhalika, wajumbe wa Baraza la Usalama walisisitiza umuhimu wa kuharakisha upelekaji wa vikosi mseto vya ulinzi wa amani vya UNAMID katika Darfur, na walipendelea kuona yale makundi yote yanayohasimiana yanashirikiana, kidhati, na UM pamoja na Umoja wa Afrika kuyatekeleza mapendekezo haya."