Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

'Ufunguo wa kuyafikia Malengo ya Milenia umo mikononi mwa wanawake', anasihi NKM

'Ufunguo wa kuyafikia Malengo ya Milenia umo mikononi mwa wanawake', anasihi NKM

Mapema wiki hii, Naibu KM wa UM, Asha-Rose Migiro aliwahutubia wanachama wa Baraza la Marekani juu ya Uhusiano wa Kimataifa (Council on Foreign Relations) liliopo mjini New York, ambapo alisailia mada iliotilia mkazo kaulimbio isemayo ‘wanawake ndio wenye ufunguo wa kuyafikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs)kwa wakati na kupunguza umasikini na hali duni kwa nusu, itakapofika 2015.”

Naibu KM alionya ya kuwa vitendo vya ubaguzi wa mpangilio, unaoendelezwa katika nchi masikini dhidi ya watoto wa kike na pia wanawake, ni hali ambayo haitoyoyawezesha Mataifa haya kutimiza malengo ya kupunguza ufukara na hali duni kwa umma masikini katika 2015.

Alisema NKM kwamba tusisahau watoto wa kike na wanawake ndio fungu lenye kujumuisha asilimia kubwa ya watu masikini na wale wanaokabikliwa na matatizo ya njaa duniani. Kadhalika, aliendelea kutahadharisha, ni watoto wa kike ndio wanaowacha masomo katika skuli za msingi kwa kiwango kikubwa zaidi kushinda watoto wa kiume; na wakati huo huo asilimia kubwa ya watoto wa kike na wanawake ndio wenye kuathiriwa zaidi na virusi vya UKIMWI.

Vile vile Naibu KM alibainisha ya kuwa mifumo ya kisheria iliopo sasa hivi ulimwenguni, haina uwezo unaoridhisha, kushughulikia masuala yanayohusu haki za wanawake.

Kwa kulingana na bayana hii, ndipo Naibu KM Migiro alitilia mkazo umuhimu na ulazima wa jamii ya kimataifa kutekeleza, kwa haraka zaidi, lengo nambari tatu linalohusu Maendeleo ya Milenia, yaani lile lengo la kuwapatia wanawake fursa na madaraka ya kumudu mambo yao wenyewe, binafsi, na pia kuweka usawa wa kijinsia, hali kadhalika.

Vile vile Naibu KM alisisitiza kwenye risala yake juu ya wajibu wa walimwengu kuhakikisha uongozi wa wanawake kwenye shughuli za uchumi unakuzwa, na wanawake huwa wanapatiwa hifadhi na ulinzi wa kisheria, dhidi ya lile janga karaha la kutumia mabavu dhidi yao.

Naibu KM Asha-Rose Migiro alikhitimisha risala yake kwa kusema kwamba anaunga mkono ile rai ya kuanzisha “taasisi moja imara itakayojihusisha na masuala ya kijinsia itakayopewa nguvu na uwezo” wa kuunganisha mifumo iliopo hivi sasa katika UM, kupigania haki za wanawake na, hatimaye, kuwasilisha usawa wa kijinsia kote ulimwenguni.

Huyu ni AK nikiripoti kutoka Redio ya UM jijini New York.