Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KM ahutubia Mkutano wa OIC

KM ahutubia Mkutano wa OIC

KM wa UM Ban Ki-moon leo alihudhuria Mkutano wa siku mbili wa Umoja wa Nchi za KiIslam (OIC) unaofanyika mjini Dakar, Senegal. Kwa mujibu wa Msemaji wa UM, KM Ban aliwasili Dakar Ijumatano ambapo alikutana kwa mashauriano na KM wa Umoja wa OIC, Ekmeleddin Ihsanoglu na walishauriana juu ya uwezekano wa kuyasuluhisha yale matatizo yanayohusu Kosovo, ukaliaji mabavu wa Israel katika maeneo ya WaFalastina, pamoja na kusailia matatizo ya ugaidi, chuki za kibaguzi dhidi ya WaIslam, na vile vile kuzingatia suala la uhuru wa mawazo na kujieleza.~

Alionya KM kwamba hali katika Mashariki ya Kati bado ni ngumu na ni ya mashaka, hususan katika eneo la Tarafa ya Ghaza, na aliisihi Israel pamoja na Serikali ya Mamlaka ya Wafalastina kuchukua hatua za dharura kujaribu kuupatia umma wa Ghaza faraja na nafuu kutokana na maafa na maumivu waliokabiliwa nayo sasa hivi, na kuwahakikishia matumaini mema kimaisha.

Kadhalika, KM aligusia kwenye hotuba yake umuhimu wa kulihitimisha kwa taratibu za kuridhisha tatizo sugu la kuchagua raisi katika Lebanon; na kudokeza kuhusu hali katika Iran na Iraq, pamoja na kuzungumzia umuhimu wa kukamilisha ule mradi wa kupeleka vikosi mseto vya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika katika Darfur (UNAMID) na kuupatia umma wa huko hifadhi bora. Vile vile aliihimiza jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi zake zitakazosaidia kutupatia suluhu imara kwenye mgogoro wa mataifa jirani ya Chad na Sudan ili kudumisha amani kieneo.