UNHCR imeanzisha rasmi mradi wa kuwarudisha Burundi, kutoka Tanzania, wahamiaji wa 1972

14 Machi 2008

Mnamo tarehe 10 Machi (2008) Kamishna Mkuu wa Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji, Antonio Guterres alimaliza ziara ya siku nne katika Tanzania baada ya kukutana na Raisi Jakaya Mrisho Kikwete kwa mazungumzo na mashauriano. Kabla ya hapo Guterres alishiriki kwenye huduma za kuanzisha rasmi mradi wa miaka miwili wa kukhitimisha lile tatizo la wahamiaji 218,000 wa kutoka Burundi, waliohamia Tanzania katika 1972 kukimbia machafuko yaliozuka nchini mwao wakati huo.

Mwisho wa wiki iliopita Guterres alikuwa miongoni mwa waheshimiwa kadha walioshuhudia operesheni za kuwarejesha makwao, fungu la kwanza la wahamiaji 255 wa Burundi, kutokea ile kambi ya Kitumba iliopo jimbo la Tanzania magharibi. Wahamiaji hawa walipelekwa kwenye bandari ya Kigoma kwa njia ya treni, na baadaye walsafirishwa kwa magari kuelekea kwenye maskani yao nchini Burundi.

Kwenye tafrija hizo za uhamisho Guterres alitoa mwito maalumu ulioitaka jamii ya kimataifa kuonesha ushikamano thabiti na serikali, pamoja na umma wa Tanzania, ili waweze kulipatia hili tatizo sugu la wahamiaji wa Burundi katika Tanzania, suluhu inayoridhisha. Alikumbusha kwamba operesheni ya kuwarejesha wahamiaji wa Burundi makwao ni mradi muhimu kabisa unaoendelezwa na UNHCR barani Afrika kwa mwaka huu. Lengo hakika la mradi huu, alitilia mkazo Guterres, ni kuwasaidia wahamiaji 46,000 kurejea makwao Burundi, kwa khiyari. Kuhusu wale wahamiaji waliosalia 172,000 wa Burundi waliopo katika taifa hilo la Afrika Mashariki, UNHCR imeripoti kuwa itajitahidi kuwahudumia, kwa nguvu moja - kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania - kuwapatia uraia, kwa kuambatana na taratibu, kanuni na sheria za Tanzania.

Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu Guterres, kadhia zote hizi hazitofanikiwa kukamilishwa kama inavyopasa, bila ya kufadhiliwa msaada maridhawa kutoka wahisani wa kimataifa. Ikumbukwe kwamba katika mwezi Februari UNHCR ilianzisha kampeni maalumu ya kuchangisha dola milioni 34 za kuendesha shughuli hizi za uhamisho, na imeahidiwa kufadhiliwa, hivi sasa, dola milioni 9 na wahisani wa kimataifa.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter