Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KM ameshtumu vikali mashambulio ya walinzi wa amani Kosovo

KM ameshtumu vikali mashambulio ya walinzi wa amani Kosovo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amechukizwa sana na kulaumu vikali mashambulio ya kutumia nguvu yaliofanywa na waandamanji wa KiSarbia Ijumatatu katika mji wa Mitrovica, Kosovo Kaskazini, dhidi ya polisi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Utawala wa Muda Kosovo (UNMIK) pamoja na vikosi vya usalama vya mataifa ya Ulaya, KFOR.

Vurugu hili lilizuka baada ya polisi wa kimataifa kujaribu kulidhibiti jengo la mahakama liliotekwa nyara wiki iliopita na magenge yenye ghasia na fujo. Tukio hilo lilisababisha watu karibu 150 kujeruhiwa, na raia mmoja wa Ukraine anayefanya kazi na Shirika la Umoja wa Mataifa la UNMIK aliuawa kutokana na majeraha aliyoyapata kwenye misongamano hiyo.

Kwenye risala aliyoitoa KM Ban juu ya suala hilo, kwa kupitia msemaji wake, alitoa nasaha kwa jamii zote zinazohasimiana katika Kosovo kujitahidi “kuonyesha uvumilivu wa kiutu na utulivu” ili kukabiliana na matatizo yao, na hali ya kutofahamiana, kwa taratibu za amani.