Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM imetangaza huzuni kubwa kwa mauaji ya madereva wanaohudumia chakula Sudan

UM imetangaza huzuni kubwa kwa mauaji ya madereva wanaohudumia chakula Sudan

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti kusikitishwa na kushtushwa sana na ile taarifa iliyothibitisha madereva watatu walioajiriwa na UM Sudan kuhudumia misaada ya kiutu waliuawa hivi karibuni. Ijumamosi, dereva mmoja anayeitwa Mohamed Ali alipigwa risasi na kuuawa na washambuliaji wasiojulikana, na walimjeruhi vibaya msaidizi wake pale walipokuwa kwenye barabara inayoelekea Nyala, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini.

Mjumbe mkaazi wa WFP katika Sudan, Kenro Oshidari alishtumu vikali kwamba uharamia kama huu ni vitendo karaha “visiokubalika abadan” na jamii ya kimataifa, na ni lazima vikomeshwe haraka. Oshidari alikumbusha vile vile ya kuwa madereva wanaoendesha magari yanayosafirisha misaada ya kuhudumia mahitaji ya kiutu, inafaa ieleweke shughuli zao hazifungamani kamwe na upande wo wote unahasimiana kieneo; na mashambulio dhidi ya aina yeyote dhidi yao hudhuru zaidi ule umma usio hatia muhitaji ambao jamii yakimataifa inawajibika kuwapatia msaada wa dharura wa chakula kunusuru maisha.