Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Balozi wa Tanzania katika UM afafanua maana ya Siku ya Kuwakumbuka Waathiriwa wa Utumwa Duniani

Balozi wa Tanzania katika UM afafanua maana ya Siku ya Kuwakumbuka Waathiriwa wa Utumwa Duniani

Tarehe 25 Machi iliadhimishwa kwenye Makao Makuu na UM, kwa mara ya kwanza kihistoria, kuwa ni Siku ya Kumbukumbu za Kimataifa kwa Waathiriwa wa Utumwa na Biashara ya Utumwa katika Ngambo ya Bahari ya Atlantiki. Kwenye taadhima za siku hiyo kulifanyika warsha maalumu kuzingatia \'athari na makovu ya utumwa kwa binadamu\'; na vile vile kuliandaliwa maonyesho na tafrija aina kwa ina za kukumbusha umma na kuwaelimisha kuhusu msiba na madhara yalioletwa na utumwa.

KM wa UM Ban Ki-moon alihutubia kikao maalumu cha kimataifa kilichoitishwa kuiheshimu siku hiyo, kikao ambacho kiliandaliwa na Wanachama wa Jumuiya ya Mataifa ya Karibian, Umoja wa Afrika pamoja na Idara ya Habari ya UM kwa Umma (DPI). Kwenye hotuba yake KM Ban alisema anatumai juhudi za kimataifa za kukumbushana juu ya “maovu na ukatili mkubwa kabisa wa kihistoria wa utumwa” zitatumiwa pia kusaidia kuuhamasisha ulimwengu kutetea wenziwao walionaswa kwenye utumwa mambo leo unaoendelezwa kwenye karne yetu ya sasa, mathalan, kama kutetea kwa niaba ya ule umma uliotekwa nyara na kutoroshwa makwao na kupelekwa maeneo ya kigeni kufanya vibarua vya lazima na visivyolipwa.

Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika UM, Balozi Augustine Mahiga, naye vile vile alizungumzia kikao hiki maalumu kwa niaba ya Umoja wa Afrika, ilivyokuwa taifa lake ni Mwenyekiti wa Umoja huo kwa hivi sasa. Baada ya tafrija hizo nilipata fursa ya kufanya mahojiano na Balozi Mahiga katika ofisini mwake kuzingatia umuhimu wa hii Siku ya Kumbukumbu za Kimataifa kwa Waathiriwa wa Utumwa.

Sikiliza dokezo ya mazungumzo hayo kwenye idhaa ya mtandao.