KM atoa wito unaohimiza mchango maridhawa kwa vikosi vya UNAMID Darfur
Baada ya kuripoti kwenye kikao cha faragha mbele ya Baraza la Usalama juu ya mizozo iliozuka barani Afrika hivi karibuni, KM Ban Ki-moon alikutana na waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu na aliwaambia kwamba wakati umewadia kwa yale mataifa yalioshadidia kupelekwa vikosi vya ulinzi wa amani Darfur, kutekeleza ahadi ya kuipatia UM zana na vifaa vinavyohitajika haraka kuhudumia operesheni zake katika eneo husika la Sudan, hususan ndege za helikopta na vile vile vifaa vinavyohusikana na huduma za usafiri. Kadhalika KM alisema vikosi mseto vya UM na UA kwa Darfur, au vikosi vya UNAMID vinahitajia kuongezewa wanajeshi ziada haraka iwezekanavyo pamoja na vifaa vya kuendesha shughuli zake kwa mafanikio.