Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma za amani na kiutu za UM katika Kenya

Huduma za amani na kiutu za UM katika Kenya

Ripoti za UM wiki hii zimethibitisha ya kuwa hali ya usalama Kenya, inaendelea kuwa tulivu, kufuatia wiki kadha za machafuko na vurugu liliofumka katika sehemu mbalimbali za nchi baada ya siotafahamu kuzuka juu ya matokeo ya uchaguzi uliofanyika Disemba mwaka jana.

Uhamisho huu wa wahamaji wa IDPs umeonekana kujiri zaidi kwenye maeneo ya kati na magharibi, na athari zake zimekutikana hasa kwenye majimbo ya Nyanza na Magharibi ambapo huduma za afya na ilimu haziwezi tena kumudu mahitaji kwa sababu ya ongezeko la wahamiaji wapya. Kadhalika, inakhofiwa pindi mtiririko huu wa wahamiaji wa IDPs utaendelea, kuna hatari ya kukabiliwa na tatizo la chakula maana akiba iliopo kwa sasa kieneo haiwezi kutosheleza mahitaji ya mfumko wa wahamiaji ziada wa IDPs.

Timu ya Mashirika Wakazi ya UM imeripoti kwamba kambi darzeni mbili ziada kwenye jiji la Nairobi zimeshapokea wahamiaji wa IDPs 12,000 na kuwapatia makazi ya muda. Vile vile tumearifiwa na Ofisi ya UM-NBI, ya kuwa kunaandaliwa mradi maalumu wa dharura wa kuwasaidia wahamiaji wa IDPs 15,000 kupata mastakimu ya muda katika eneo la Kasarani, liliopo kwenye vitongoji vya Nairobi.

JINGLE (09”)

RIJAL:Machafuko ya karibuni ya Kenya yameripotiwa kusababisha matatizo ya uchumi, halkadhalika, katika soko la kimataifa.

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limebashiria kwenye ripoti iliyotolewa Alkhamisi kwamba bei ya chai katika 2008 itaendelea kupanda kwenye soko la kimataifa kutokana na uhaba wa bidhaa hiyo, hali ambayo vile vile imeathirika na machafuko yaliotukia Kenya karibuni. Kwa mujibu wa FAO Kenya inakifu asilimia 10 ya bidhaa ya chai katika soko la kimataifa.

Kwa mujibu wa FAO, biashara ya chai duniani haijabadilika sana katika miaka ya karibuni. Mathalan, kuanzia 2006 jumla ya biashara ya chai katika soko la kimataifa ilitulia kwenye kiwango cha tani milioni 1.55 (moja, laki tano na elfu khamsini) ambapo lile pengo liliosababishwa na upungufu wa bidhaa hiyo kutokea Kenya na pia Indonesia lilitoshelezwa na chai iliyotokea Sri Lanka na Vietnam, mataifa ambayo katika kipindi cha karibuni yameongeza uzalishaji wa chai kwenye maeneo yao.

Ripoti ya FAO itawakilishwa kwenye Warsha utakaofanyika Dubai kuanzia tarehe 19 hadi 20 Februari Kuzungumzia Biashara ya Chai Duniani.