Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kikao cha dharura cha BU kuzingatia Kosovo

Kikao cha dharura cha BU kuzingatia Kosovo

Ijumapili alasiri wajumbe wa Mataifa 15 Wanachama wa Baraza la Usalama (BU) walikusanyika kwenye kikao cha dharura, na cha faragha, hapa Makao Makuu kilichoitishwa na Shirikisho la Urusi kuzingatia mvutano uliozuka kimataifa juu ya tangazo la uhuru liliotolewa na jimbo la Kosovo, katika Serbia. ~~

Naibu Balozi wa Marekani, Alejandro Wolf aliwaambia wanahabari, kufuatia majadiliano ya faragha kwenye Baraza, kuwa Serikali yake inaunga mkono uamuzi wa Kosovo na kusisitiza kwamba hatua hii haimaanishi jumuiya ya kimataifa inahalalisha kitendo cha aina hii baadaye.

KM wa UM Ban Ki-moon aliwadhihirishia waandishi habari wa Makao Makuu kwamba yeye bado anaendelea kushauriana na Mjumbe wake Maalumu kwa Kosovo, Joachim Rucker, ambaye alimhakikishia hali sasa hivi kwenye jimbo la Kosovo, kwa ujumla, ni shwari, licha ya kuripotiwa kutukia mripuko katika eneo la kaskazini la Mitrovica. KM aliziomba pande zote husika na suala la Kosovo kujiepusha na vitendo vyote vya uchochezi, au kutoa zile kauli za chuki ambazo huenda zikazusha vurugu na kuhatarisha usalama na amani ya Kosovo na eneo zima jirani.

Kwa mujibu wa KM Ban, UM utaendelea kutekelza majukumu iliyodhaminiwa na Baraza la Usalama katika Kosovo hadi pale wajumbe wa Baraza watakapoamua kurekibisha huduma za ulinzi wa amani katika eneo hilo.

Mamlaka ya Kosovo, jimbo la Serbia liliotangaza uhuru wa upande mmoja Ijumapili Februari 17 2008, yanasimamiwa na UM tangu mwezi Juni 1999.

Tutakupatieni ripoti ziada kutoka kikao cha hadhara cha Baraza la Usalama kitachofanyika Ijumatatu.