Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

'Wadudu si kero bali hurutubisha lishe', yanasihi FAO

'Wadudu si kero bali hurutubisha lishe', yanasihi FAO

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limeripoti kwamba aina 1,400 za wadudu wanaokutikana kwenye misitu ya dunia huliwa na wanadamu. FAO imetayarisha pamoja na Chuo Kikuu cha Chiang Mai,Thailand wiki hii warsha wa siku tatu ambapo wataalamu wa kimataifa wanazingatia uwezekano wa kuanzisha biashara ya wadudu, kwa chakula, katika maeneo ya Asia na ukanda wa Pasifiki, ikiwa miongoni mwa juhudi za kupunguza tatizo la njaa duniani. Wadudu wanaoliwa na wanadamu wamegunduliwa kurutubisha pakubwa lishe. ~

Miongoni mwa mamia ya aina za wadudu walioripotiwa ni chakula cha wanadamu, wanaopendwa zaidi na watu wamegawika katika sehemu nne:sehemu ya kwanza inajumuisha aina ya mbawakawa; sehemu ya pili,hukusanya wadudu chungu, siafu, nyuki na nyigu; fungu la tatu ni la panzi na senene; na aina ya nne hujumuisha nondo na vipepeo. Asilimia kubwa ya wadudu wanaoliwa na wanadamu huvunwa kutoka misituni.