Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti kuwa ulimwengu unakabiliwa na ukosefu wa wahudumia afya milioni 4, na eneo lenye upungufu mkubwa zaidi ni bara la Afrika ambalo pekee linahitajia kidharura wafanyakazi milioni moja ziada ili kuweza kuyafikia malengo ya maendeleo na afya bora kama ilivyodhamiriwa na Nchi Wanachama. Kuanzia tarehe 2 hadi 7 Machi jumuiya ya kimataifa itakusanyika mjini Kampala, Uganda kuhudhuria mkutano wa kimataifa utakaojumuisha wataalamu wa serikali, wale wa kutoka sekta ya afya, vyuo vikuu na pia mashirika yasio ya kiserekali, ili kuzingatia hatua za kuchukuliwa kipamoja kusuluhisha tatizo la upungufu wa wahudumia afya duniani.

Baada ya kuwasilisha ripoti juu ya usalama wa mradi wa nishati ya nyuklia wa Iran mbele ya Bodi la Magavana wa Shirika la UM juu ya Matumizi ya Amani ya Nishati ya Nyuklia (IAEA) Mkurugenzi Mkuu wake, Mohamed ElBaradei aliwaambia waandishi habari mjini Vienna juu ya kupatikana “maendeleo ya kutia moyo” na mafanikio katika kufafanua yale masuala yaliokuwa na utata siku za nyuma kuhusu miradi ya nishati ya nyuklia ya Iran. Hata hivyo, ElBaradei alitahadharisha ya kuwa bado kuna vizingiti fulani vimebakia kuhusu matokeo ya utafiti wa Iran juu ya silaha za kinyuklia.