Mashirika ya UM yanuia kukomesha ukeketaji wa watoto wa kike duniani

28 Februari 2008

Mashirika kumi ya Umoja wa Mataifa - yakijumuisha yale mashirika yanayoshughulikia huduma za kudhibiti UKIMWI (UNAIDS), kuimarisha miradi ya maendeleo (UNDP), maendeleo ya elimu, sayansi na utamaduni (UNESCO), Kamisheni ya Maendeleo ya Uchumi kwa Afrika (UNECA) na Mfuko wa Kudhibiti Idadi ya Watu Duniani, UNFPA; na vile vile yale yanayohusika na ulinzi wa haki za binadamu (OHCHR), huduma za wahamiaji (UNHCR), mfuko wa maendeleo ya watoto (UNICEF), mfuko wa maendeleo ya wanawake (UNIFEM) na pia afya ya kimataifa (WHO)- Ijumatano yametoa ripoti ya pamoja iliyoahidi kuchangisha kila juhudi ili kukomesha ile tabia haribifu ya kutahiri watoto wa kike, katika kipindi cha kizazi kimoja, pote duniani.

Taarifa ya mashirika ya Umoja wa Mataifa ya kutahiri watoto wa kike iliwasilishwa mbele ya kikao cha khamsini na mbili cha Kamisheni ya Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Wanawake (CSW) na Naibu Katibu Mkuu Asha-Rose Migiro, ambaye kwenye risala yake mkutanoni alisisitiza ya kuwa walimwengu wanaweza kulikamilisha lengo la mashirika ya UM pakichukuliwa hatua za pamoja.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa inakadiriwa watoto wa kike na wanawake baina ya milioni 100 hadi milioni 140, wameshatahiriwa hivi sasa ulimwenguni, na kila mwaka watoto wa kike milioni 3 wengineo hukabiliwa na hatari ya kutahiriwa katika sehemu kadha wa kadha za dunia.

Sikiliza habari kamili kwenye idhaa ya mtandao

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter