Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM yaunga mkono mwafaka wa Kenya kuunda Serikali ya Muungano

UM yaunga mkono mwafaka wa Kenya kuunda Serikali ya Muungano

KM Ban Ki-moon Alkhamisi alitoa taarifa rasmi iliyoyapongeza “Maafikiano ya Ushirikiano wa Serikali ya Muungano” nchini Kenya, mapatano ambayo anaamini yatakapokamilishwa yatasaidia kuwasilisha suluhu ya kuridhisha kwa makundi yote yanayohusika na mzozo uliolivaa taifa lao katika wiki za karibuni.

Ijumaa kwenye mazungumzo na waandishi habari mjini Geneva, Veronique Taveau, msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa juu ya Maendeleo ya Watoto (UNICEF), aliarifu kwamba mapatano hayo ya kisiasa yalikuwa ni ushindi mkubwa kwa watoto wa Kenya. Alisema UNICEF inaunga mkono mapatano ya kuunda serikali ya mpito kwa sababu yanabashiria alama njema itakayowapatia watoto matumaini na maisha tulivu katika siku zijazo.