Uchumi wa dunia kwa 2008 unakabiliwa na hatari ya mzoroto, kuonya UM
Wiki hii UM uliwasilisha ripoti maalumu katika Makao Makuu New York na vile vile kwenye ofisi zake ziliopo mjini Geneva, ambayo ilizingatia na kutabiri hali ya uchumi duniani katika 2008. Ripoti ilitayarishwa shirika na Idara ya UM juu ya Masuala ya Uchumi na Jamii (DESA) pamoja na Shirika la Maendeleo na Biashara (UNCTAD).
Kadhalika Sundaram alisema utafiti wao umegundua kunyemelea mporomoko wa shughuli za uchumi Marekani, hali ambayo inakhofiwa huenda ikasababisha matumizi ya wateja kuteremka na kuathiri uchumi wa kimataifa, kwa ujumla, kwa sababu ya matatizo yanayotokana na watu wanaoshindwa kulipa mikopo yao ya nyumba, kadhia ambayo hutumiwa na wanauchumi kuashiria mwelekeo wa shughuli za kiuchumi kitaifa.
Kuhusu Mataifa ya Afrika, uchumi huko uliongezeka kwa nguvu katika 2007, na unabashiriwa kuendelea kupanuka katika mwaka huu kwa kiwango cha asilimia 6, licha ya kuwa ni nchi chache tu zitakazofaidika, kihakika, barani humo na ongezeko la huduma za kiuchumi katika 2008.