Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Mnamo 2007 Shirika la Mfuko wa UM Kudhibiti Idadi ya Watu (UNFPA) limepokea mchango wa dola milioni 419 kutoka mataifa 181 kutumiwa katika kuongoza shughuli zake za mwaka, mchango ambao ulikiuka rikodi ya msaada uliopokewa miaka iliopita.

Balozi Leo Merores wa Haiti ameteuliwa kuwa Raisi wa 64 wa Baraza la UM juu ya Maendeleo ya Uchumi na Jamii (ECOSOC), na Baraza vile vile limewachagua Manaibu-Raisi wanne kuitumikia taasisi kwa mwaka 2008.

Mnamo mwisho wa Januari mji wa Bali, Indonesia utakusanyisha wajumbe 1,000 kutoka mataifa 100 ziada – wakiwakilisha Serikali, mashirika ya biashara, wahudumia shughuli za usalama, waandishi habari, pamoja na waburudishaji na wasanii na pia wawakilishi wa jumuiya za kiraia – kwenye Mkutano wa UM juu ya Vita dhidi ya Ulajirushwa, ambapo pia watashauriana hatua za kuchukuliwa kipamoja kudhibiti bora karaha hii.

Mohamed ElBaradei, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Matumizi ya Amani ya Nishati ya Nyuklia (IAEA) amemamliza ziara ya karibuni Iran na alifanikiwa kufikia maafikiano ya kuridhisha mjini Teheran na viongozi wa taifa, akiwemo Ayatullah Ali Khamenei na Raisi Mahmoud Ahmadinejad, ambao walishuariana kuhusu taratibu za kuthibitisha kihakika dhamira ya operesheni za viwanda vya nishati vya nyuklia katika Iran.

KM Ban Ki-moon alipohutubia Mkutano wa Taasisi ya Ushirikiano wa Tamaduni na Mila Tofauti katika mji wa Madrid, Uspeni wiki hii aliwanasihi walimwengu kujiepusha na ile tabia ya utovu wa kutostahamiliana kitamaduni, na alipendekeza watu wasiolingana kitamaduni na kimila kurekibisha tafauti zao kwa majadiliano, kadhia ambayo anaamini ndiyo pekee ya salama na yenye natija na uwezo wa kujenga mafahamiano ya kuridhisha dhidi ya maudhiano yenye kuvuka mipaka ya kiutu.