Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KM ahimiza utulivu wa kisiasa katika JAK

KM ahimiza utulivu wa kisiasa katika JAK

Ripoti ya karibuni ya KM Ban Ki-moon kuhusu hali katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (JAK) imeelezea kwamba matayarisho yanaendelezwa kuitisha mjadala wa kisiasa utakaojumuisha vikundi vyote kuzingatia mzozo uliosababishwa na vitendo vya uchokozi wa waasi katika maeneo ya kaskazini-magharibi na kaskazini- mashari ya nchi.

Kuhusu matatizo ya kiutu ripoti ya KM ilisema hali imetulia baada ya maafikiano ya amani kutiwa sahihi baina ya Serikali na kundi la waasi la UFDR mwezi Aprili, na baada ya raia waliong'olewa kutoka makazi yao kwa sababu ya mapigano walipoanza kurejea vijijini kwao. Kadhia hii imeteremsha idadi ya wahajiri wa ndani ya nchi (IDPs) kutoka 65,000 hadi 45,000, na wakati huo huo idadi ya wahamiaji ambao bado wamebakia katika kambi ziliopo taifa jirani la Cameroon ni sawa na watu 45,000.

KM Ban aliyataka makundi yote husika kushiriki katika majadiliano ya kizalendo yaliokusudiwa kukomesha duru ya ugeugeu wa kisiasa na vurugu ambalo linaendelea kudhuru taifa kijumla. KM aliahidi kuwa UM upo tayari kutoa mchango wote unaotakiwa kurudisha utulivu na amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.