Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mataifa ya KiAfrika na FAO yaahidi kuimarisha elimu vijijini

Mataifa ya KiAfrika na FAO yaahidi kuimarisha elimu vijijini

Mataifa 11 ya KiAfrika, yalikutana karibuni mjini Rome, Utaliana kwenye Makao Makuu ya Shirika la UM la Chakula na Kilimo (FAO) na yaliafikiana kushiriki kwenye ule mradi wa kuimarisha elimu ya msingi vijijini, kwa dhamira ya kusaidia wakazi wa maeneo hayo kujipatia ujuzi wa kupiga vita, kwa mafanikio, ufukara, matatizo ya njaa, utapia mlo na kutojua kusoma na kuandika. Maafa haya ya kijamii huathiri zaidi mataifa ya Afrika yaliopo kusini ya Sahara.

Kwa mujibu wa takwimu za UM, asilimia 70 ya idadi ya watu Afrika huishi katika vijiji. Miongoni mwa mataifa yatakayoshiriki kwenye mradi huu wa FAO ni pamoja na Ethiopia, Kenya, Msumbiji, Bukini, Uganda, Afrika Kusini na Tanzania.