Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa Bali kuzingatia mabadiliko ya hali ya hewa waonesha dalili za kutia moyo - kumbukumbu

Mkutano wa Bali kuzingatia mabadiliko ya hali ya hewa waonesha dalili za kutia moyo - kumbukumbu

Kuanzia mwanzo wa wiki, wajumbe zaidi ya 10,000 wakiwakilisha nchi wanachama karibu 190, pamoja na waangalizi wa mashirika ya kiserekali na yasio ya kiserekali, na vile vile waandishi habari, walikusanyika Kisiwani Bali, Indonesia na kushiriki kwenye mijadala, itakayoendelea kwa majuma mawili, hadi Disemba 14, kuzingatia ajenda ya msingi wa mashauriano kuhusu Mkataba mpya wa kuimarisha udhibiti bora wa mabadiliko ya hali ya hewa duniani katika siku za usoni, hususan baada ya Maafikiano ya Kyoto kukamilisha muda wake katika 2013. Mashaurianio ya kimataifa kuhusu Mkataba mpya baada ya Maafikiano ya Kyoto yanapangwa kukamilishwa 2009.

Achim Steiner, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) alinakiliwa akisema kwamba mabadiliko ya hali ya hewa husababisha athari mbaya zinazodhuru na kuleta hasara kimaisha. Lakini alikumbusha vile vile ya kuwa tafiti za kimataifa zimethibitisha kihakika kwamba athari za mabadiliko ya hali ya hewa zina natija zake pia, kwa kumaanisha tatizo hili husaidia kuzalisha viwanda vipya vinavyotakikana kudhibiti muongezeko wa hali ya joto duniani, kadhia ambayo huzalisha ajira kwa mamilioni ya watu.

Yvo de Boer, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi inayosimamia Utekelezaji wa Maafikiano ya UM Kudhibiti Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani (UNFCCC) aliwaambia waandishi habari waliokusanyika Bali, Indonesia kwamba anaamini mijadala ya Mkutano wa Bali yanaashiria mazingira ya kutia moyo, na aliwakumbusha wawakilishi wa nchi wanachama kwamba wasisahau macho yote ya umma wa kimataifa yameelekezewa Bali, na jukumu walionalo hivi sasa ni kuhakikisha wanafikia maafikiano ya kuridhisha, yatakayoleta natija maridhawa kwa wote, pote ulimwenguni.