Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ya hapa na pale

Ya hapa na pale

Miaka 15 baada ya kuanzishwa majadiliano ya kusailia taratibu za kuhifadhi misitu ya dunia na uharibifu, Baraza Kuu la UM limefanikiwa kupitisha azimio la khiyari litakalosaidia kuimarisha hifadhi bora ya hii rasilmali ya kimataifa.

Kadhalika FAO imeripoti ya kuwa kilimo cha umwagiliaji maji kinahitajia kurekibishwa kwenye mashamba ya mpunga yaliopo mataifa ya Asia, kitendo ambacho kikikamilishwa kitasaidia kupunguza sumu ya asenia (arsenic) iliyosakama kwenye chemchemi za maji yaliopo chini ya ardhi, na kwenye michirizi iliopitia majabali yenye sumu ya asenia.

KM Ban Ki-moon amepongeza na kuunga mkono kupitishwa kwa lile azimio la khiyari na Baraza Kuu ambapo ilipendekezwa kwa Mataifa Wanachama kuakhirisha adhabu ya kifo, na alisisitiza ni matumaini yake adhabu hii itakomeshwa na kufutwa kabisa kutoka sheria za kimataifa.

[na mwishowe] Mkutano wa Awali wa Taasisi ya Ushirikiano wa Kitamaduni unaoandaliwa na Serikali ya Uspeni, unatarajiwa kufanyika kwenye mji wa Madrid mwezi Januari (15-16) 2008 kwa makusudio ya kutafuta uwiano mpya wa kuziba pengo la kutofahamiana kitamaduni, pengo ambalo linaendelea kupanuka na kufarakanisha mataifa mbalimbali ulimwenguni, na kikao hicho kinatazamiwa kusaidia katika uimarishaji wa mafahamiano mazuri baina ya mataifa yenye tamaduni tofauti.