Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamati ya CTC yasailia udhibiti wa ugaidi

Kamati ya CTC yasailia udhibiti wa ugaidi

Kamati ya Baraza la Usalama dhidi ya Ugaidi au Kamati ya CTC ilipohitimisha mijadala ya siku tatu kwenye Makao ya UM mjini Nairobi Kenya, ilitoa taarifa ya pamoja na pia mpango wa utendaji, uliowakilisha karibu darzeni tatu ya mashirika ya kikanda na kimataifa, maafikiano ambayo yalilenga juhudi za kuimarisha uwezo wa nchi zao kuwanyima magaidi fursa ya kuvuka mipaka kihorera.

Vikao vya mkutano wa Nairobi vilisailia mada kadha wa kadha, hasa kuhusu viwango vya kimataifa na zile taratibu za kutumiwa kuimarisha usalama wa bidhaa zinazosafirishwa ndani na nje ya nchi, kulinda usafiri wa anga kwa raia na pia kuhifadhi uchukuzi kwa njia ya bahari.

Miongoni mwa mashirika ya kimatafa yaliosimamia na kuongoza majadiliano yalijumuisha Shirika la Kimataifa Juu ya Usafiri wa Ndege za Kiraia (ICAO), Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR), Shirika la Polisi wa Kimataifa dhidi ya Uhalifu (INTERPOL) pamoja na Wakurugenzi Watendaji wa Kamati ya Baraza la Usalama dhidi ya Ugaidi au Kamati ya CTC.