Ripoti ya UNESCO kuzingatia athari za mapigano katika ilimu

9 Novemba 2007

Utafiti ulioendelezwa na Shirika la UM juu ya Ilimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuhusu namna huduma za ilimu zinavyoathirika kutokana na mapigano imeonesha wanafunzi, walimu na vile vile wanazuoni mara nyingi hushambuliwa kihorera na makundi yanayohasimiana, kwa makusudi bila ya kisingizio.

Ripoti imependekeza kwa jamii ya kimataifa kubuni hatua za kisheria, mapema iwezekanavyo, ili kulinda na kutunza taaluma ya siku za usoni kwa watoto wanoishi kwenye maeneo ya mapigano.

Brendan O’Malley, Mwandishi Mkuu aliyeongoza utafiti wa UNESCO alipokutana na waandishi habari wa kimataifa hapa Makao Makuu aliwabainishia orodha ya mashambulio ambayo hupaliliwa sekta ya ilimu kwenye vurugu la vita: alizungumzia namna wanafunzi wanavyotekwa nyara, au kushambuliwa kwa mabomu na mara nyengine hulazimishwa kusiriki kwenye mapigano wangali bado wana umri mdogo. O’Malley vile vile alisema uchunguzi wao umefichua kwamba walimu huuliwa makusudi ndani ya maskuli; na mara nyengine skuli hugeuzwa kuwa kambi za kijeshi au hubomolewa kwa kupigwa makombora na mizinga, na mara nyingi wanachama wa vyama vya walimu hupotea na kutojulikana walipo.

Kwa mujibu wa takwmiu rasmi za kimataifa asilimia 40 ya wanafunzi milioni 77 wasiohudhuria skuli huishi kwenye maeneo yenye vita na mapigano. Jamii ya kimataifa, hususan Baraza la Usalama, ilitakiwa kuanzisha hatua za utendaji za pamoja, ikijumuisha kampeni za kuteteta haki za binadamu, na pia kuanzisha utaratibu wa kutunza takwimu za kimataifa za kuiwasaka wale wote wanaotuhumiwa kuendeleza jinai hii na kuhakikisha wanafikishwa mahakamani kukabili haki.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter