Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DR Congo: UNICEF na washirika wake wasaidia kuwaokowa watoto 230 kutoka kwa wanamgambo

DR Congo: UNICEF na washirika wake wasaidia kuwaokowa watoto 230 kutoka kwa wanamgambo

Shirika la watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF pamoja na shirika la Save the Children wamefanikiwa kuwaokoa watoto 230 kutoka kwa wanamgambo wa kundi la Mayi Mayi huko Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, lakini wanasema kuna kazi kubwa ya kufanywa kukomesha kuandikishwa watoto katika vita hasa majimbo yenye ghasia ya Kivu nchini humo.

Taarifa ya UNICEF inaeleza kwamba, watoto hao waliweza kuachiliwa huru kutoka kundi la Mayi Mayi kaskazini na kusini mwa Kivu mnamo siku chache zilizopita kutokana pia na msaada wa afisi ya Umoja wa Mataifa huko DRC MONUC na kufuatia kampeni kabambe ya kupinga uandikishaji na utumiaji watoto katika makundi ya kijeshi. Shirika hilo limetoa wito kwa makundi yote ya waasi kuwachilia huru mara moja watoto na kuwakabidhi kwa mpango wa kuwapokonya silaha na kuwarudisha katika maisha ya kiraia nchini humo DDR.