Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali Usomali inawatia wasiwasi mkubwa wajumbe wa Baraza la Usalama

Hali Usomali inawatia wasiwasi mkubwa wajumbe wa Baraza la Usalama

Baada ya mashauriano kukamilishwa ndani ya Baraza la Usalama juu ya hali katika Usomali, Balozi Marty Natalegawa wa Indonesia, Raisi wa Baraza kwa mwezi Novemba, aliwasilisha kwa waandishi habari taarifa ya pamoja, kwa niaba yawajumbe wa Baraza yenye kuelezea wasiwasi mkuu ulioivaa jamii ya kimataifa juu ya kuharibika kwa hali ya kisiasa, usalama na vile vile mazingira ya kiutu nchini Usomali.

Baraza la Usalama limetilia mkazo umuhimu wa “kuandaliwa mradi wa dharura utakaozingatia uwezekano wa kupeleka vikosi vya ulinzi wa amani vya UM katika Usomali.”

Kadhalika, Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti ya kuwa idadi ya watu waliong’olewa makwao kutokana na mfumko wa vurugu na mapigano yalioshtadi hivi karibuni Usomali, imepindukia watu milioni moja; na imeripotuiwa kwamba asilimia 60 ya umma huo ilijumuisha wakazi wa mji mkuu wa Mogadishu waliojikinga na athari mbaya za mazingira yaliokosa nidhamu na sheria.