Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Shirika la UM juu ya Maendeleo ya Ilimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limewasilisha ripoti mpya yenye kuthibitisha maendeleo ya kutia moyo katika miaka 10 iliopita ambapo idadi ya watoto wanaohudhuria skuli za msingi iliongezeka, hususan miongoni mwa watoto wa kike, na pia kuliongezeka kwa fedha zinazotumiwa kimataifa katika sekta ya ilimu, licha ya kuwa ilimu ya watu wazima bado iliendelea kuzorota takriban duniani kote.

Kampeni ilioanzishwa mwaka jana na Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) ya kupandisha miti bilioni moja kabla ya mkutano wa Bali kufanyika mwezi Disemba imeripotiwa kufanikiwa baada ya mti wa bilioni moja kusajiliwa kuoteshwa nchini Ethiopia, juhudi ambazo zilipongezwa hadi na mwanaharakati wa mazingira, na pia mtunukiwa wa Zawadi ya Nobel kwa Amani, Wangari Maathai.

[na hatimaye] Alkhamisi, tarehe 29 Novemba, iliadhimisha na UM kuwa ni Siku ya Ushikamano wa Kimataifa na Umma wa Falastina, siku ambayo maofisa kadha wa UM, pamoja na wajumbe wa kimataifa walitoa risala zenye kuhimiza kwamba wakati umewadia wa kutekeleza kwa vitendo zile ahadi zilizotolewa kimataifa za kuleta suluhu ya amani Mashariki ya Kati baina ya Israel na Falastina.