Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Manadalizi ya vikosi mseto vya UM/UA katika Darfur yasonga mbele

Manadalizi ya vikosi mseto vya UM/UA katika Darfur yasonga mbele

Kundi la kwanza la wahandisi wa kijeshi 135 kutoka Uchina wamewasili karibuni mjini Nyala, katika Darfur Kusini, wakijumuisha furushi la mchango wa UM kusaidia Operesheni za Umoja wa Afrika za AMIS katika Darfur. Vikosi hivi vya Uchina vitahudumia kazi muhimu ya kutayarisha makazi kwa vikosi mseto vya ulinzi wa amani vya UM na UA vya UNAMID.

Mjumbe Maalumu wa KM kwa Darfur, Jan Eliasson pamoja na Naibu KM juu ya Operesheni za Amani za UM, Jean-Marie Guehenno walipozungumzia mbele ya wajumbe wa Baraza la Usalama, kwenye kikao cha hadhara, juu ya matayarisho ya operesheni za UNAMID katika Darfur walionya kwamba kuna hatari ya kutokamilisha kwa wakati idadi ya vikosi mseto vya UM na Umoja wa Afrika kwa Darfur kwa sababu Serekali ya Sudan imezusha vizingiti kadha wa kadha, na pia Mataifa Wanachama bado hayajachangisha misaada muhimu ya kijeshi inayotakiwa kuanzisha operesheni za ulinzi wa amani katika Darfur. Wakuu hawa wa UM walionya ya kwamba hali hii ni ya hatari, hasa ilivyokuwa wiki chache zimesalia kabla ya madaraka ya operesheni za amani katika Darfur kukabidhiwa Shirika mseto la UNAMID.

Bado tukizungumzia Sudan, Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) limefanikiwa kuwapatia ajira watu 7,000 nchini kutokana na ule Mradi wa Kufufua na Kurekibisha Huduma za Kiuchumi nchini Sudan. Kadhia hii itasaidia kukamilisha kwa wakati baadhi ya yale Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) katika Sudan.

Mjumbe Maalumu wa KM kwa Sudan, Ashraf Qazi alikutana majuzi na viongozi wa Sudan, akiwemo pia Naibu Raisi Ali Osman Taha na alisailia nawo taratibu za kufufua tena na kuimarisha, kwa wakati, yale maafikiano ya amani yaliotiwa sahihi na viongozi wa wawakilishi wa majimbo ya kusini na kaskazini ya nchi, baada ya uhasama wa muda mrefu kusitishwa.