Walimwengu watambua mchango wa watu wazee katika maendeleo

5 Oktoba 2007

Tarehe 01 Oktoba iliadhimishwa na UM kuwa ni ‘Siku Kuu ya Watu Wenye Umri Mrefu/Watu Wazee’ na kulitolewa mwito maalumu ulioyahimiza mataifa yote wanachama kuandaa miradi ya kizalendo, kwa dhamira ya kuwapatia umma wa kimataifa wenye umri wa miaka 60 na zaidi, wanaotafsiriwa kama watu wazee, pensheni ya kudumu maridhawa itakayowasaidia kuishi vizuri kama raia wengine wenziwao.

Takwimu za UM zinaashiria katika 2050 idadi ya watu wazee duniani itaongezeka mara mbili zaidi, kwa asilimia 22, kwa kulingana na kiwango cha 2006 cha asilimia 11. Muongezeko huu, tumearifiwa, utakithiri zaidi katika nchi zinazoendelea, nchi ambazo ndipo watakuwa wakiishi asilimia 80 ya watu wazee katika miaka ya ijayo.

Muktadha wa mwaka huu kuheshimu ‘Siku Kuu ya Watu Wazee’ unahimiza: “Zingatia Halisi Vizingiti, Natija Bora na Fursa Adhimu za Kimaisha kwa Watu Wazee.” Muktadha huu unatambua umuhimu wa ushirkiano wa wadau wote husika – kuanzia Mataifa Wanachama, mashirika ya NGOs, UM na mashirika yake na pia watu wazee – kwenye majadiliano ya kutekeleza mapema Mpango wa Utendaji wa Kimataifa wa Madrid, ulioandaliwa kuboresha maendeleo na maisha ya watu wazee katika karne ya 21.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter