Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

Rachel Mayanja, Mshauri Maalumu wa KM kuhusu Masuala ya Kijinsia na Maendeleo ya Wanawake amependekeza kwa jamii ya kimataifa kubuniwe kanuni za kukabiliana na vitendo haramu vya kutumia mabavu na kujamii kwa nguvu wanawake kwenye mazingira ya vita, na alitaka vitendo hivi vitafsiriwe kama uvunjaji sheria wa kiwango cha juu wenye kuvuka mipaka ya maadili ya kiutu.~

Baraza la Usalama limehimiza Mataifa Wanachama, pamoja na UM yenyewe, kuwahusisha zaidi wanawake katika kufanya maamuzi kwenye sera za kimataifa, na kutaka kuchukuliwe hatua maalumu zitakazohakikisha wanawake wanapatiwa hifadhi kinga dhidi ya utumiaji wa nguvu na mabavu dhidi yao kwenye mazingira ya vita.

Ripoti ya Kamisheni ya UM juu ya Maendeleo ya Uchumi Afrika (ECA) imethibitisha kuwepo mafanikio kwenye juhudi za mataifa tajiri kusamehe madeni yao dhidi ya nchi za Afrika; na wakati huo huo wahisani wa kimataifa wameonekana bado kuwa wagumu katika kuzitekeleza zile ahadi walizotoa kabla za kufadhilia misaada ya kukuza maendeleo katika Afrika.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya hatari ya virusi vya homa ya mafua ndege vya H5N1 kujirekibisha na kufumka kuwa janga la homa ya maambukizo dhidi ya wanadamu, hali ambayo itahitajia maandalizi kinga ya dharura dhidi ya maradhi.