Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa DPI/NGOs kuzingatia taathira za uchafuzi wa hali ya hewa duniani

Mkutano wa DPI/NGOs kuzingatia taathira za uchafuzi wa hali ya hewa duniani

~Mkutano shirika wa mwaka wa Idara ya Habari kwa Umma ya UM (DPI) pamoja na jumuiya za kiraia (NGOs) ulianza kikao chake cha siku tatu katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa wiki hii. Mada ya mwaka huu ilisema “Mabadiliko ya Hali ya Hewa: Namna Yanavyotuathiri Sisi Sote.”

Mkusanyiko wa mwaka huu, uliotayarishwa na Idara ya DPI kwa ushirikiano a mashirika yasio ya kiserekali (NGOs) umejumuisha wajumbe 2,000 ziada pamoja na washiriki wa kutoka jumuiya za kiraia waliowakilisha sehemu kadha wa kadha za dunia, kwa makusudio ya kuzingatia tatizo la athari za mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni, suala ambalo KM Ban Ki-moon aliwania kuwa ndio moja ya mada atakayoipa umuhimu wa kiwango cha juu kabisa.

Naibu KM Asha-Rose Migiro kwenye hotuba ya ufunguzi, kwa niaba ya KM, alisisitiza kwamba tatizo la athari ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani “huhitajia mchango wa kimataifa kulitatua; juhudi ambazo zitawajibu serekali, sekta ya binafsi na jumuiya za kiraia kujumuika kudumuisha mageuzi ya kuridhisha yenye natija kwa wote.”

Raisi wa Baraza Kuu la UM, Sheikha Haya Rashed al-Khalifa risala yake vile vile ilinasihi kwamba athari za mabadiliko ya hali ya hewa hazitoweza kudhibitiwa kihakika mpaka pale patakapowasilishwa “mapinduzi ya tabia na mawazo” ya “kizalendo”, na kuhakikisha tunazishirikisha jamii zetu zote katika huduma za kutambua huduma zinazofaa kupewa umuhimu na kutekelezwa, kwa minajili ya natija ya umma wote wa kimataifa.