Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Tarehe 10 Septemba iliadhimishwa na UM kuwa ni ‘Siku ya Kuzuia Vitendo Karaha vya Kujiua Duniani’, hasa ilivyokuwa takwimu za wataalamu wa kimataifa zimethibitisha kuwa katika kila nukta 30 mtu mmoja huwa anajiua ulimwenguni kwa sababu kadha wa kadha.

Shirika la UM juu ya Matumizi ya Nishati ya Nyuklia kwa Huduma za Amani (IAEA) limetoa ripoti mpya yenye kuwatahadharisha walimwengu na kuwahimiza kuongeza uangalifu wao dhidi ya biashara haramu ya vifaa vya kutengenezea silaha za kinyuklia, hususan baada ya vitendo hivi kuonekana kuongezeka katika 2006.

Risala ya KM Ban Ki-moon mbele ya Mkutano wa Wadau Walioridhia Mkataba wa UM dhidi ya Hatari ya Kuenea kwa Majangwa, ambao unafanyika mji wa Madrid, Uspeni wiki hii, ilisisitiza kwamba vile “vitisho pacha” vya mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na kutanda kwa majangwa ni matatizo yanayohitajia suluhu ya dharura ili kunusuru umma wa kimataifa na madhara haribifu.

Kuanzia Ijumaa watu milioni 35, katika sehemu kadha wa kadha za dunia, wanatarajiwa kushiriki, kwa hiyari,kwenye shughuli zinazoungwa mkono na UM zinazojulikana kama ‘Huduma za Mwisho wa Wiki Kuondosha Uchafu Duniani’, huduma ambazo huhusika na uzoaji takataka, kuotesha miti na kutunza maji, shughuli zilizokusudiwa kuboresha maisha na afya na kutunza mazingira.

[na hatimaye] Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limewasilisha ripoti mpya inayothibitisha kupungua kwa vifo vya watoto wadogo chini ya umri wa miaka mitano, kwa kiwango kikubwa katika 2006, kima ambacho kwa mara ya kwanza jumla ya vifo iliteremka chini ya watoto milioni 10, tukilinganisha na iadi ya watoto waliosajiliwa 1990 ambapo jumla ya vifo hivyo ilikuwa watoto milioni 13.