Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Masaibu ya wahamaji wa Pembe ya Afrika yaomba suluhu ya kimataifa

Masaibu ya wahamaji wa Pembe ya Afrika yaomba suluhu ya kimataifa

Shirika la Kimataifa juu ya Wahamaji (IOM) limeripoti kuwa linahitajia kufadhiliwa msaada wa dharura najamii ya kimataifa, utakaoliwezesha kununua vifaa vya kusajili na kuhifadhi takwimu za wale wahamaji na watu wenye kuomba hifadhi ya kisiasa kutoka eneo la Pembe ya Afrika, ambao wameanza kuwasili kwa wingi katika Yemen hivi karibuni baada ya kuvuka Ghuba ya Aden.

Kadhalika wiki hii Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti kuanzishwa tena vitendo vya ukatili na wale maharamia wenye kuvusha magendo watu baina ya Usomali na Yemen. Kwa mujibu wa UNHCR watu 12 walifariki wiki iliopita na kutoswa baharini baada ya kuteswa kutokana na vitendo vya kutisha kabisa, ambapo inasemekana wahamaji watano walipigwa marungu na kuchomwa visu na maharamia na baadaye kutupwa majini, na sita wengine walifariki kwa sababu ya kiu na kukosa pumzi walipofungiwa chini ya mashua.