Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchina itajitahidi kujihusisha kikamilifu kuleta suluhu maridhia Darfur

Uchina itajitahidi kujihusisha kikamilifu kuleta suluhu maridhia Darfur

Mjumbe wa Uchina juu ya Suala la Darfur, Balozi Liu Guijin alizuru Makao Makuu mwanzo wa wiki na alikutana na wawakilishi wa jamii ya kimataifa pamoja na KM Ban Ki-moon. Kadhalika alichukua fursa hii na kufanya mazungumzo na Idhaa ya Redio ya UM ambapo alihojiwa na Fan Xiao wa vipindi vya Kichina. Balozi Liu aliombwa aelezee sababu hasa zilizoifanya Serekali ya Uchina kuamua kuteua Mjumbe Maalumu kushughulikia suala la Darfur?:

“Inafaa tukumbushane hapa kwamba suala la Darfur ni suala muhimu sana; kwa sababu Darfur ni eneo lenye vurugu la kisiasa linalomurikwa, takriban, na kila mtu ulimwenguni. Kwa hivyo, Serekali ya Uchina inasisitiza ni muhimu kabisa kujumuika na jamii ya kimataifa ili kutafuta suluhu ya msingi kuhusu Darfur inayoridhisha. Madaraka hasa nilionayo ni kuwasiliana na wote wahusika na suala hili, ikijumuisha mataifa ya magharibi, na vile vile wadau wengine muhimu, mathalan, Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa, na kushauriana nawo kimawazo, ili kuendeleza mafahamiano ya pamoja katika kutafuta suluhu ilio sawa juu ya mzozo huu. Hilo hasa ndio jukumu langu. Ama jukumu jengine nililokabidhiwa nalo na Serekali yangu ni kuelimisha walimwengu kuhusu mwelekeo hakika juu ya sera ya Uchina kwa suala la Darfur; kuelezea kile kilichofanywa na Uchina kusukuma mbele juhudi za amani na mipango ilioandaliwa kurudisha utulivu na amani katika siku za usoni; yaani kuhakikisha umma wa kimataifa una ufahamivu mzuri zaidi kuhusu sera hakika ya Uchina juu ya Darfur.”

Kadhalika Balozi Liu alisema kwamba baada ya yeye kuteuliwa kuwa Mjumbe Maalumu wa Uchina kwa Darfur alibahatika kupata fursa ya kulizuru eneo la mgogoro mara mbili, na alitembelea sehemu za kaskazini na kusini ya Darfur, na pia kuzuru zile kambi za wahamiaji wa ndani ya nchi (IDPs). Vile vile kwenye ziara yake alisema alikutana na viongozi wa Sudan pamoja na wawakilishi wa zile jamii zilizofungamana na mzozo wa Darfur, vikao ambavyo, alitilia mkazo, vilimwezesha kubadilishana mawazo kuhusu hatua zitakazofaa kutumiwa kipamoja kurudisha utulivu na amani ya eneo. Alisema Serekali ya Uchina inaunga mkono, bila pingamizi, mazungumzo ya kuendeleza majadiliano ya upatanishi kati ya makundi yote husika na mzozo wa Darfur, na pia kuunga mkono rai ya kupelekwa vikosi mseto vya kimataifa kutoka Umoja wa Afrika (AU) na UM, na anaamini ilivyokuwa Uchina ina uelewano mzuri zaidi na Serekali ya Sudan ana matumaini makubwa mchango wao utathaminiwa.